The text is included here to aid students using the 2001 edition of the text with the original audio based on the 1988 edition. Copyright Sharifa Zawawi.
Watalii wa Kiamerika wamefika Dar es salaam. Wamekodi kiongozi mjini wa kuwaonyesha mahali muhimu
katika mji huu. Dar es salaam ni mji mkuu wa Tanzania.
James: Tutafurahi kuzunguka mjini na kuona majenzi na vitu muhimu. Je u tayari?
Kingozi: Ndiyo, hii ndiyo kazi yangu. Twendeni njia hii.
Janet: Kwani njia hii kuna nini?
Kingozi: Mmeona jumba lile?
Janet: Jumba gani lile?
Janet: Lile ni Ikulu. Jumba analokaa Rais wa nchi hii.
Janet: Jengo zuri kabisa na anapata hewa safi ya pwani.
Jerry: Je lile nalo ni jenzi gani?
James: Lile ni Bunge.
Jerry: Tunaweza kuchungulia ndani?
Kingozi: Ndiyo. Ni ruhusa kwa mtu yoyote kutembelea Bungeni.
James: Kuna wanasiasa wangapi hapa Tanzania?
Kingozi:Sina hakika lakini wengi. Nadhani hawapungui wanasheria mia moja na hamsini.
Janice:Wanasiasa wa huku wanachaguliwa na wananchi au wanachaguliwa na Rais?
Kingozi: Wengi wanachaguliwa kwa sauti za wananchi, yaani kwa voti, lakini wachache wanachaguliwa na Bunge lenyewe na wengine wanachaguliwa na Rais.
Janice: Jenzi la Bunge limekaa mahali pazuri na safi kabisa. Tena jenzi la kisasa.
Kingozi: Lile mbele yetu ni kanisa la katoliki, kuna makatoliki wengi humu mjini.
James: Je, dini gani nyingine zipo Tanzania?
Kiongozi: Aa, huku kwetu kuna kila aina ya dini hasa watu wengi ama ni wakristo ama waislamu.
James: Waislamu wanaabudu ndani ya kanisa kama wakristo?
Kiongozi:La, waislamu wanaabudu ndani ya msikiti.
Jerry: Msikiti? Msikiti ni nini?
James: Kiongozi kakwambia kwamba msikiti ni nyumba ya ibada ya Waislamu. Kama ilivyo kanisa ni nyumba ya ibada ya Wakristo na hekalu ni nyumba ya ibada ya mabaniani. Zote nyumba za Mungu.
Jerry:Je upo msikiti hapa Dar es salaam?
Kiongozi: Ndiyo, ipo misikiti mingi, mingine mikubwa mingine midogo.
Janet: Naona nyumba nzuri kule, nyumba gani ee?
Kiongozi: Ile ni nyumba ya makumbusho. Makumbusho ya vitu vya kale.
Jerry: Huu ni mji wa zamani sana?
Kiongozi: Ndiyo ni mji wa kale. Nadhani mji wa Dar es salaam ulibuniwa yapata sasa karne tisa au kumi hivi. Jina lake la zamani lilikuwa ni Mzizima.
James: Hili jina la Dar es Salaam maana yake nini?
Kiongozi: Hili ni neno la Kiarabu na maana yake ni mahali pa salama. Jina lake la pili zamani lilikuwa bandari salama, maana bandari ya salama lakini sasa jina hili hulisikii tena ila kwa nadra.
Janet: Jina zuri kabisa pwani yake ni shwari na salama, jina lililofanana kabisa.
Jerry: Kuna majumba mazuri njia hii ya Pwani?
Kiongozi: Majumba haya ni wizara mbalimbali za serikali, jumba hili kwa mfano ni wizara ya Sheria, lile pembezoni ni wizara ya Fedha, na kule ni wizara ya wizara ya Elimu; wizara ya ukulima iko mbali kidogo hatuwezi kuiona hapa tuliposimama. Mtaa huu ndiyo makao makubwa ya serikali.
Jerry: Naona ngoma na watu wamejipanga kando ya njia na wamechukua bendera, kuna nini leo ee?
Kiongozi: Leo atafika Rais wa Mali kwa ziara rasmi ya siku tatu. Tazameni upande ule, mmeona? Zile ni motokari za mawaziri zinakwenda kiwanja cha ndege kumpokea Rais wa Mali; labda Rais wetu naye vilelvile atapita sasa hivi kwenda kumpokea mgeni wetu mtukufu. Akipita Rais motokari yake itakuwa imeandamwa na askari juu ya pikipiki. Leo kutakuwa na sherehe na ngoma kutwa.
James: Wananchi wa Tanzania wanaonyesha kuwa wana furaha katika nyuso zao, tena wana adabu na urafiki, unasemaje kiongozi?
Janet: Bwana we tumechoka mwendo wa miguu, bora tupumzike mkahawani kidogo tule askIrimu, kisha tuendelee na matembezi yetu kwa motokari.
James: Mwanamke wee! Pesa za teksi ziko wapi?
Janet: Kumradhi...nimechoka, hata ukinichinja katu siendi tena kwa miguu pesa unazo tele! Wacha ugumu wako James.
Jerry: Kweli baba, sote tumechoka, twende kwa gari.
James: Vema, vema, nyinyi mtakalo lazima mpate. Mmezoea raha lazima mjifundishe kutaabika vilevile maana maisha hayaendi namna moja siku zote. Leo hivi kesho hivi.
Kiongozi: Mnasemaje, si bora tutembelee kijiji cha Oysterbay? Kuna ufuo mzuri wa bahari na labda mtapenda kuogelea
Janet: Vizuri sana nimetamani kuyaoga maji ya bahari ya Bara Hindi... Naona wanawake wamevaa nguo ndefu nyeusi na wengine wamefunika nyuso zao. Kwa nini ee?
Kiongozi: Wale wanawake wa kiislamu wanavaa mabuibui, wasichana wa kiislamu wanaokwenda shule hawavai tena mabuibui.
James: Jua kali sana tumetembea muda mrefu, bora tupumzike mkahawani tule kidogo chakula cha mchana kabla ya kuendelea na matemebezi yetu, wasemaje mzee Kiongozi?.